Kylian Mbappe Asema “Wale kina Ronaldo ni magwiji”
Mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe, amekataa kulinganishwa na magwiji wa soka kama Cristiano Ronaldo na Ronaldo Nazario licha ya kuwa karibu kuvunja rekodi zao za mabao katika msimu wake wa kwanza na klabu hiyo.
Mbappe, mwenye umri wa miaka 26, amefunga mabao 30 katika mechi 43 alizocheza msimu huu. Hii inamfanya awe mbele ya Ronaldo Nazario, aliyefunga mabao 29 katika mechi 43 kwenye msimu wake wa kwanza na Real Madrid baada ya kujiunga kutoka Inter Milan mwaka 2002. Pia, Mbappe yupo nyuma kwa mabao matatu tu kumfikia Cristiano Ronaldo, aliyefunga mabao 33 katika mechi 35 kwenye msimu wake wa kwanza baada ya kujiunga na Real Madrid mwaka 2009.
Akizungumza baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Villarreal, ambapo alifunga mabao yote mawili, Mbappe alisema: “Hao ni magwiji ambao walikuwa na zama zao. Ni kitu muhimu, lakini hilo ni suala la namba. Kama nitafunga mabao mengi kuliko Ronaldo na Cristiano, hiyo haina maana kuwa mimi ni mkubwa, huu ndiyo kwanza ni msimu wangu wa kwanza.”
Aliongeza kuwa lengo lake kuu ni kuisaidia timu kushinda mataji: “Kufunga ni jambo muhimu, lakini yatakuwa muhimu zaidi kama tutashinda La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Copa del Rey.”
Real Madrid ipo katika nafasi nzuri ya kushinda mataji matatu msimu huu, ikiwa inaongoza La Liga, ipo nusu fainali ya Copa del Rey baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Real Sociedad katika mechi ya kwanza, na imefuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo itakutana na Arsenal.
Mabao Mengi Katika Msimu wa Kwanza na Real Madrid:
- Cristiano Ronaldo – mabao 33
- Ruud van Nistelrooy – mabao 33
- Kylian Mbappe – mabao 31
- Ronaldo Nazario – mabao 30
- Jude Bellingham – mabao 23
Mbappe anaendelea kuonyesha kiwango cha juu katika msimu wake wa kwanza na Real Madrid, lakini anakiri kuwa bado ana safari ndefu kufikia hadhi ya magwiji kama Ronaldo na Cristiano Ronaldo.